Pages

Pages

Pages

Friday 6 December 2013

KILA SAFARI INA RAHA NA KARAHA ZAKE!

 Najiandaa kuondoka. Hapa ni Lake Manyara Tented Camp, ndipo nilipojilaza. Sasa niko tayari kwa safari ya kwenda Serengeti baada ya kuzuru Hifadhi ya Ziwa Manyara.

 Niko na mtangazaji maarufu wa Radio Ebony FM ya Iringa, Raymond Francis.
 Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, Ibrahim Petro Ninga, akiwaeleza wanahabari walioko ziarani mafanikio na changamoto zinazoikabili hifadhi hiyo.
 Mkutano na wanahabari ukiendelea.
 Naam, tuko kwenye geti la kuingilia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
 Mimi na Mwenyekiti wa Iringa Press Club (IPC), Frenk Leonard.
 Baadhi ya wanahabari walioko ziarani wakiwa katika picha ya 'pamoja'.
 Ofisa wa Mamlaka ya Ngorongoro akitoa maelezo kwa wanahabari walioko ziarani.
Hapa sasa tunaingia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Mengi nitawaletea jioni.

Ndugu zangu,
Tumeingia mjini Mugumu, makao makuu ya wilaya ya Serengeti mkoani Mara majira ya saa 6:30 usiku huu tukitokea Manyara. Pamoja na uchovu mwingi nilionao, nimeona ni vyema nisiwaache bila kuwaeleza yaliyojiri.
Tumeondoka mahali tulipojilaza pale Mto wa Mbu kwa usiku wa kuamkia jana majira ya saa 2:00 asubuhi. Kwa kuwa juzi hatukufanikiwa kuonana na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ziwa Manyara Ibrahim Petro Ninga, ilibidi tupite kwanza tupate kumuuliza mambo machache kuhusiana na hifadhi hiyo, lakini ambayo yanaweza kusaidia nasi wanahabari wa Nyanda za Juu Kusini tukautangaza utalii katika kanda hiyo inayoonekana kuwa nyuma katika suala zima la utalii nchini.
Baada ya mazungumzo yetu yaliyochukua takriban dakika arobaini, tukaendelea na safari yetu. Kifungua kinywa tulipata pale Karatu, lakini tukachelewa kidogo kutokana na kujipanga kwa safari ndefu ya kuja Serengeti.
Tulifika kwenye geti la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kama saa 4:30 hivi. Hapa pia ofisa wa Mamlaka hiyo akatupatia maelezo kuhusiana na eneo la hifadhi ya Ngorongoro, ambayo ndiyo pekee inayoruhusu binadamu kuchangamana na wanyamapori huku wakifanya shughuli zao za kiuchumi.
Wanaoruhusiwa kuishi katika eneo hili ni Watanzania wa jamii ya Kimasai – tena wanatakiwa wawe waliozaliwa eneo hilo. Hawa ndugu zetu wanatajwa kwamba ni rafiki wakubwa wa mazingira haya kwa sababu wamekuwepo kwa miaka mingi na wamekuwa wakitunza mazingira pamoja na raslimali zilizopo bila kuleta athari zozote.
Naam, baada ya hapo majira ya saa 5:24 tukaianza safari yetu ndefu kuelekea Serengeti. Njiani tumeona wanyama mbalimbali wakiwemo Pofu, Swala kwa aina zake, Pundamlia, ‘Madaktari wa Porini’ – yaani Fisi, Ngiri, na makundi ya Nyati.
Kwa kweli ilikuwa ni safari ndefu, na ukumbuke kwamba hatukupata chakula cha mchana tangu tulipoamsha kinywa pale Karatu. Hii ni kwa sababu hapo katikati hakuna sehemu ambayo unaweza kupata huduma ya chakula.
Kabla ya kuingia Seronera gari yetu ikatitia kidogo pembeni mwa barabara kutokana na utelezi kwa vile mvua ilikuwa ikinyesha. Hakuna aliyesalia ndani ya gari isipokuwa binti mdogo na mama yake. Wote tukateremka na kuanza kuisukuma gari itoke. Ungetuona jinsi tunavyohangaika, wallah ungecheka na kutuhurumia pia. Gari ikanasuka, si penye nia pana njia jamani? Tena ukizingatia wakati huo giza limeingia halafu mko hifadhini, bila kusahau kwamba Simba anaweza kutokea wakati wowote na upande wowote.
Mwendo wa basi letu huwezi kuufanyanisha na magari yale ya kitalii, hasa kwa barabara yenyewe ilivyo, hivyo tukaingia Seronera majira ya saa 1:26 usiku. Hapa tukapata chakula katika Hoteli ya Impala. Tunawashukuru wenyeji wetu TANAPA kwa kutufanyia mpango mapema, maana ule mtikisiko wa safari uliacha matumbo yetu yakiwa yametepeta.
Saa 2:30 ndipo tulipoondoka Seronera kuelekea Mugumu, ambako ndiko tukakojilaza. Tayari wenzangu wamelala, lakini mimi nimeona siwezi kulala mpaka niwaeleze yaliyojiri.
Kutoka Seronera hadi Mugumu ni umbali wa kilometa 90, hivyo kwa mwendo wa gari yetu wa kilometa 20 mpaka 25 kwa saa kutokana na ubovu wa barabara, ilitulazimu kutumia muda wa saa 4 hivi hadi kufika Mugumu.
Lakini wakati tulipotoka tu pale Seronera tukakutana na wafalme wa mwitu, Simba. Walikuwa kama watatu hivi na tuliwatambua kwa mbali kutokana na macho yao yanayong’ara gizani. Dada mmoja akatania baada ya kuona mmoja wa simba hao akipiga miayo huku akijifanya kama hajaona chochote kwamba gari isimame ili watu ‘wakachimbe dawa’! Nani ateremke wakati anamuona simba jike akipiga miayo ya njaa!
Naam, tumesinzia tukaamka, safari ikiwa inaendelea mpaka saa 6:30 tulipingia Mugumu. Nimefikia katika hoteli ya Giraffe, ni nzuri kwa kweli. Kesho, nina maana ya leo hii asubuhi, tutarudi tena katika Hifadhi ya Serengeti tuendelee na ziara yetu ya mafunzo. Usingizi inabidi tuuweke kando kwa muda, maana kilichotuleta ni muhimu pia.
Wasaalam,

Daniel Mbega.

No comments:

Post a Comment